WATU 13 wamefariki dunia na wengine kujeruiwa katika ajali ya basi lililokuwa linatoka soko la Awasi Kisumu kuelekea Nairobi nchini Kenya.
Kwa mujibu wa duru za Kenya ajali hiyo ilitokea majira ya saa tano na nusu, usiku wa kumkia leo.
Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Kisumu, Benson Maweu amethibitisha kutokea ajali hiyo na kusema kuwa, miili 13 imetolewa katika eneo na ajali na kwamba, kuna watu wengine kadhaa waliojeruhiwa katika ajali hiyo.
Kamanda huyo wa polisi amesema kuwa, basi hilo lilikuwa likisafiri kutoka Kisumu kuelekea Kericho.
Imeelezwa kuwa, ajali hiyo ilihusisha basi hilo na lori moja na kwamba, miongoni mwa waliofariki dunia yumo mtoto mmoja.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, dereva wa lori ni miongoni mwa watu waliofariki dunia katika ajali hiyo na kwamba majeruhi wa ajali hiyo wamepelekwa hospitali kwa ajili ya matibabu.