Katibu wa Itikadi na Uenezi wa ACT- Wazalendo, Ado Shaibu amechukuliwa na Jeshi la Polisi kwa Mahojiano alipokuwa katika Makao Makuu ya chama hicho, Kijitonyama jijini Dar es salaam akiandaa mkutano wa kiongozi mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe kwa ajili ya kuzungumza na waandishi habari.

Jeshi la Polisi Kanda Maalim ya Dar es Salaam lilifika katika makao makuu ya chama hicho na kuzuia mkutano huo ambao ulitarajiwa kufanyika leo Ijumaa Agosti 16,2019 saa 5 asubuhi.
Polisi waliwasili Makao Makuu ya chama hicho na kumhitaji kiongozi yoyote wa chama baada ya kumkosa Zitto Kabwe.
“Ndugu waandishi huu mkutano usubiri kwanza, kwa hiyo ninawaomba mtawanyike mara moja,” alisema askari mmoja.
Wakati waandishi wakitawanyika aliwasili Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu ambaye walimchukua na kuondoka naye kwa ajili ya mahojiano.