Wizara ya Mambo ya Ndani ya Israel imetangaza kuwa waziri mkuu Bw. Benjamin Netanyahu amewazuia wabunge wanawake wawili wa kwanza wa kiislamu kuchaguliwa kuwa wabunge wa Marekani, Rashida Tlaib na Ilhan Omar, kuingia nchini mwake kwa madai kuwa wanapambana na Israel.

Uamuzi huo umekuja saa chache baada ya Rais Donald Trump kuandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa Omar na Tlaib wanaichukia Israel na Wayahudi.
Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani Bibi Nancy Pelosi amekosoa vikali hatua hiyo na kusema imeonyesha dalili ya udhaifu na kupunguza uadilifu wa Israel.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini Marekani, viongozi hao wawili walikuwa na ziara ya kikazi Jumapili hii, ambayo pia ingelijumuisha wao kufika eneo tata la Temple Mount mjini Jerusalem, linalotambuliwa na Waislamu kama Haram al-Sharif.

Pia walikuwa na mpango wa kukutana na wanaharakati wa amani wa Israel na Palestina na kusafiri hadi ukingo wa Magharibi wa Jerusalem katika miji ya Bethlehem, Ramallah na Hebron.