Mahakama ya Rufani imetupilia mbali ombi la kuangaliwa upya hukumu ya kunyongwa, aliyohukumiwa Christopher Bageni, ambaye alifungua shauri hilo kutaka afutiwe adhabu hiyo, kwa kosa la mauaji ya wafanyabiashara watatu wa madini mkoani Morogoro.
Uamuzi wa kutupilia mbali maombi hayo ya Bageni ulioandaliwa na jopo la majaji watatu wa mahakama hiyo waliosikiliza maombi hayo, umetolewa leo Jumatano, Agosti 14, 2019 na Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama ya Rufani, Elizabeth Mkwizu.
Jopo la majaji hao waliosikiliza na kutoa uamuzi wa maombi hayo namba 63 ya mwaka 2016 ni Stella Mugasha (kiongozi), Ferdinarnd Wambali na Rehema Kerefu.
Kwa uamuzi huo ambao ndio wa mwisho, sasa Bageni hana namna nyingine ya kufanya kwani hakuna ngazi nyingine ya mahakama nchini wala hatua nyingine ambayo anaweza kuichukua kuupinga.
Kwa sasa atasubiri tu utekelezaji wake huku akiombea neema ya rais wa awamu ya sasa au awamu zijazo kumsamehe ama kumwachia huru au kumbadilishia adhabu pengine kuwa ya kifungo kwa mamlaka yake kikatiba kama ataguswa au kuona kuna sababu ya kufanya hivyo.