Televisheni ya taifa ya Iran imeripoti kuwa kiongozi mkuu wa kidini nchini humo ametoa wito wa kuungwa mkono kwa waasi wa Houthi wa nchini Yemen dhidi ya muungano wa kijeshi unaongozwa na Saudi Arabia ambao amesema unalenga kuitenganisha nchi hiyo.

Ayatollah Ali Khamenei ametoa matamshi hayo wakati alipokutana hapo jana mjini Tehran na Mohamed Abdul Salam ambaye ni msemaji wa waasi wa Houthi.
Khamenei amesema Saudi Arabia, Muungano wa Falme za kiarabu na wale wanaowaunga mkono wanalenga kuiharibu Yemen ambayo ametaka isimame imara dhidi ya njama hizo.
Muungano wa kijeshi unaongozwa na Saudi Arabia ambao unajumuisha pia Falme za Kiarabu umekuwa ukipambana na waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran katika eneo la Kaskazini ya Yemen tangu Machi 2015 ili kuilinda serikali ya rais Abdo Rabbo Mansur Hadi.