Waziri wa Nishati nchini Tanzania, Dk Medard Kalemani amesema Rais wa Tanzania, John Magufuli keshokutwa Ijumaa Julai 26, 2019 ataweka jiwe la msingi katika Mradi wa kufua umeme wa megawati 2115 wa Rufiji ‘Stigler’s Gorge’ uliopo mikoani ya Pwani na Morogoro.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Julai 24, 2019 Morogoro, Waziri Kalemani amesema tukio hilo kubwa la kihistoria kukamilika kwake kutawezesha Taifa Kuwa na umeme wa kutosha, wa uhakika, unaotabirika na hatimaye kuwa wa gharama nafuu kwa watumiaji.

Amesema wizara inawahakikishia Watanzania kuwa utekelezaji wa mradi huo ni wa kasi, weledi na nidhamu na hiyo ni katika kuunga mkono juhudi za Serikali inayongozwa na Rais Magufuli.

Mradi huo mkubwa wa umeme utakapokamilika unatarajia kutumia kiasi cha Sh6.5 trilioni ambazo ni fedha za Serikali ya Tanzania.