Iran inasaema imewakamata majasusi 17 wanaofanya kazi katika Shirika la Ujasusi la Marekani, CIA, na wengine wamehukumiwa adhabu ya kifo.

Televisheni ya taifa ya Iran imemnukuu afisa wa wizara ya ujasusi akisema kuwa pia imelivunja genge la majasusi hao.
Afisa huyo amesema waliokamatwa wamehukumiwa adhabu ya kifo.
Tangazo hilo limetolewa miezi mitatu tangu kuzuka kwa mvutano na mataifa ya Magharibi ulioanza wakati Marekani ilipoweka vikwazo vikali kwa Iran ambavyo vilianza rasmi mwezi Mei.
Wiki iliyopita, Iran iliikamata meli ya mafuta yenye bendera ya Uingereza katika Mlango Bahari wa Hormuz, baada ya Uingereza kuikamata meli ya mafuta ya Iran kwenye pwani ya Gibraltar, Julai 4.
Haijajulikana wazi kama kukamatwa majasusi hao kunahusiana na kesi ambayo Iran ilisema mwezi Juni kuwa imegundua mtandao mkubwa wa kijasusi iliyodai unaendeshwa na CIA na kwamba majasusi kadhaa wa Marekani walikamatwa katika nchi tofauti.