Jeshi la Walinzi wa Kimapinduzi nchini Iran limesema limekamata meli yenye bendera ya Uingereza katika lango la bahari la Hormuz baada ya kukiuka sheria za kimataifa za baharini.
Hatua hii inakuja wakati kukiongezeka hali ya wasiwasi katika eneo hilo tete la bahari.
Uingereza imesema Iran imekamata meli mbili katika eneo la Ghuba huku waziri wake wa mambo ya nje Jeremy Hunt akionya hatua kali za kisasi iwapo suala hilo halitashughulikiwa mara moja.

“Kutakuwa na ‘madhara makubwa” ikiwa Iran haitaachia meli ya mafuta ya uingereza wanayoishikilia” Amesema Waziri wa mambo ya kigeni Jeremy Hunt .

”Tunajua wazi kuwa hali hii haitakuwa rahisi kuitatua, kutakuwa na madhara makubwa.

”Hatuangalii suluhu ya kijeshi.Tunatafuta suluhu ya kidiplomasia kutatua hali hii, lakini tunajua tunapaswa kushughulikia.”- Amesema

Amesema wafanyakazi ndani ya meli walikuwa wa mataifa tofauti tofauti lakini hakuna raia wa Uingereza aliyekuwa akifahamika kuwa ndani ya chombo hicho.

”Balozi wetu mjini Tehran anfanya mawasiliano na wizara ya mambo ya kigeni wa Iran kutatua hali hii na tunafanya kazi kwa karibu na washirika wetu wa kimataifa,” amesema.

Mmiliki wa meli ya Mesdar ambayo ni miongoni mwa zilizokamatwa amesema wanajeshi wenye silaha waliingia kwenye meli hiyo kwa muda kabla ya kuiruhusu kuondoka.
Tukio hili linakuja baada ya jana rais Donald Trump wa Marekani kusisitiza kwamba manowari ya Marekani iliidungua ndege ya Iran isiyokuwa na rubani iliyokuwa ikitishia usalama wa meli na wafanyakazi katika lango hilo la Hormuz.