H any Ahmed (27) ambaye ni raia wa Misri amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na shtaka moja la kutorosha madini aina ya diamond yenye thamani zaidi ya Sh. Milioni 12.

Akisoma hati ya mashtaka jana July 16, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba, Wakili wa Serikali Wankyo Simon alidai, Julai 10, mwaka huu huko katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam mshtakiwa alikutwa akisafirisha madini ya diamond yenye uzito wa carats 11:12 ambayo yana thamani ya Dora za Kimarekani 5,238 sawa na Sh. 12,050,131bila ya kuwa na kibali.

Hata hivyo, mshtakiwa hakuruhusiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kesi hiyo imeahirishwa hadi Julai 30, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa, mshtakiwa amerudishwa rumande.