Mkuu wa kundi la Hezbollah Hassan Nasrallah amesema Iran, inao uwezo wa kuiangamiza Israel iwapo vita kati ya Marekani na Iran itatokea.
Mkuu huyo wa Hezbollah amesema ni wazi Israel ambayo ni mshirika wa Marekani haiwezi kuacha kufungamana na upande wowote iwapo vita itatokea kati ya nchi hizo mbili.
Nasrallah, ambaye kundi lake linaungwa mkono na Iran ameyasema hayo katika mahojiano yake na kituo cha televisheni cha Al Manar wiki chache baada ya kuzidi kufukuta kwa mgogoro kati ya Marekani na Iran.
Ameongeza kuwa, iwapo Marekani ingejua kuwa vita dhidi ya Iran vinaweza kuiangamiza Israel, ingejitafakari upya.
Israel, imefanya mamia ya mashambulizi nchini Syria dhidi ya kile inachokiita maeneo yanayolengwa kijeshi ya Iran na Hezbollah.
Hapo jana, baraza la wawakilishi la Marekani, lilipiga kura ya kudhibiti uwezo wa Rais Trump wa kuishambulia Iran likihofia sera zake zinazoelekea kuanzisha vita visivyo vya lazima.