Rais wa Marekani Donald Trump, leo amesifia mazungumzo kati yake na rais wa China Xi Jinping na kuyataja kuwa mazuri kuliko yalivyotarajiwa, na ameahidi kusitisha kuongeza ushuru kwa bidhaa za China wakati mazungumzo kati yao yakiendelea.
Siku moja tu baada ya mazungumzo yao mjini Osaka Japan, pembezoni mwa mkutano wa kilele wa nchi wanachama wa G20, Trump ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa ubora wa mazungumzo ni muhimu zaidi kwake kuliko kasi.
Kwa hivyo hana haraka, lakini mambo yanaonekana kuwa mazuri.
Trump na Xi walikubaliana kufanya mazungumzo ya kusitisha uhasama wa kibiashara kati ya nchi zao. Trump alithibitisha kuwa Marekani imejitolea kutoongeza ushuru mpya kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka China.
Marekani na China zimekuwa kwenye mzozo wa kibiashara huku pande zote zikiongeza ushuru kwa bidhaa.