Aliyekuwa Rais wa Sudan, Omar al-Bashir amejitokeza hadharani kwa mara ya kwanza tangu kuondolewa kwake madarakani mwezi Aprili.
Bwana Bashir alikuwa akitolewa gerezani katika mji mkuu, Khartoum kwenda kwenye Ofisi ya mwendesha mashtaka ambaye alimsomea mashtaka ya rushwa yanayomkabili
Akiwa amezungukwa na askari wa usalama, Kiongozi huyo wa zamani mwenye miaka 75 alikua amevaa vazi lake jeupe na kilemba.
Bwana Bashir alipinduliwa madarakani baada ya miezi kadhaa ya maandamano nchini humo.
Waendesha mashtaka wanasema kuwa maburungutu ya fedha za kigeni yalikutwa kwenye magunia nyumbani mwake baada ya kuondolewa madarakani alikohudumu kwa takribani miaka 30.
Bashir alionekana akishuka kwenye gari kuingia kwenye ofisi ya mwendesha mashtaka, akitabasamu na kuzungumza na walinzi, lakini baadae alirejea akiwa na uso usio na furaha, Shirika la Reuters limeeleza.
Bwana Bashir pia anatakiwa na mahakama ya kimataifa, ICC, akishutumiwa kuongoza vitendo vya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binaadamu katika eneo la Darfur, shutuma ambazo amezikana.
Advertisements