Mahakama Kuu ya Tanzania imemhukumu kunyongwa hadi kufa aliyekuwa mlinzi wa shule ya Scolastica mkoani Kilimanjaro, Hamis Chacha kwa kosa la kumuua aliyekuwa mwanafunzi wa shule hiyo, Humprey Makundi.

Pia, Mahakama hiyo imemuhukumu mmiliki wa shule hiyo, Edward Shayo na aliyekuwa mwalimu wa nidhamu, Labani Nabiswa kifungo cha miaka minne jela kila mmoja wa kosa la kuficha ukweli wa mauaji ya mwanafunzi huyo.

Hukumu hiyo imetoelewa leo Jumatatu Juni 3, 2019 na Jaji Firmin Matogolo baada ya kumtia hatiani Chacha kwa kumuua kwa makusudi mwanafunzi huyo wa kidato cha pili, Makundi.

Mwanafunzi huyo aliuawa Novemba 6,2017 na baadaye mwili wake kutupwa mto Ghona, mita takribani 300 kutoka shuleni na baadae kuzikwa na Manispaa kabla ya kufukuliwa kwa amri ya mahakama.