Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, inatoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki wa Familia za Watumishi Wanane wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Mfanyakazi Mmoja wa Chama Kijamii waliofariki katika ajali ya barabarani iliyotokea tarehe 23 Februari, 2019, katika Mto Kikwawila, Wilaya ya Kilombero, Mkoani Morogoro.

Gari ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero, aina ya Toyota Land Cruiser yenye namba za usajili STK 994, waliopanda Watumishi hao ambao walikuwa Wanatekeleza Mradi wa Wizara hiyo, kwenye Halmashauri hiyo, ilikuwa inaenda Ifakara ilipofika daraja la Mto Kikwawila liliingia kwenye daraja na kutumbukia Mtoni upande wa kushoto na kusababisha vifo vya Watumishi tisa.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Kangi Alphaxard Lugola, MB, kwa masikitiko makubwa anatoa pole kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa William Lukuvi, pamoja na ndugu wa familia zote zilizopoteza wapendwa wao katika ajali hiyo.

“Natoa pole nyingi kwa Mheshimiwa Waziri Lukuvi, ndugu, jamaa na marafiki waliowapoteza wapendwa wao katika ajali hii, Mwenyezi Mungu aziweke roho za Marehemu mahali pema peponi, Amina,”.

Imetolewa na:
Meja Jenerali Jacob G. Kingu, ndc
KATIBU MKUU
23 Februari, 2019.

Advertisements