Kiongozi wa upinzani nchini DRC, Martin Fayulu amekataa juhudi za Rais mpya, Felix Tshisekedi za kutaka maridhiano, baada ya uchaguzi mkuu wa kwanza wa kidemokrasia kumalizika.
Mwito huo wamaridhiano ulitoleawa na Rais huyo mpya katika jitihada za kutafuta maridhiano ya kisiasa nchini hapa.
Hata hivyo jitiahada hizo za Rais Tshisekedi zinaonekana kugonga mwamba baada ya Fayulu kusema kuwa pale unapopewa mkono ambao ni mchafu, hupaswi kuupokea.
Kauli ya Fayulu imekuja siku chache baada ya Rais Tshisekedi kusema katika hotuba yake aliyoitoa baada ya kuapishwa kwamba nchi yake haitakuwa ni ya upande mmoja ama ukabila, huku akisisitiza kuwa tayari kukutana na wapinzani ili waweze kushirikiana kujenga Congo imara.
“Tunataka kujenga Congo imara katika utamaduni wake. Tutakuza maendeleo kwa amani na usalama. Congo ni ya kila mmoja ambapo kila mtu ana nafasi yake mwenyewe, “alisema Tshisekedi.
Fayulu alitoa kauli hiyo juzi katika mkutano wake wa kwanza tangu aliposhindwa kwenye uchaguzi wa rais uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana wakati akiwahutubia mamia ya wafuasi wake waliokusanyika mjini hapa.
Hata hivyo pamoja na kukataa wito huo wa maridhiano, kiongozi huyo aliwataka wafuasi wake wasifanye fujo wakati anapoendelea kupinga uchaguzi anaodai ulikumbwa na udanganyifu.
“Hakuna haja ya kufanya vurugu ila tutaendelea kupaza sauti zetu katika jumuiya za kimataifa ili haki ipatikane,”alisema kiongozi huyo.
Aliuhimiza Umoja wa Mataifa (UN) na wa Afrika (AU) kutopokea maagizo kutoka kwa mtu anayedai kuwa Wakongo hawakumchagua
Advertisements