Watu wanaodaiwa kuwa majambazi, wamevamia nyumba ya kulala wageni ya Malema Lodge katika mtaa wa Sinde jijini Mbeya, inayomilikiwa na Diwani Viti Maalumu (CCM), Mary Malema, kisha kufanya ubakaji kwa wahudumu na mlinzi na hatimaye kupora fedha.
Unyama huo waliufanya usiku wa kuamkia jana baada ya kuwapa ofa ya vinywaji na biskuti zinazodaiwa kuwa na dawa za kulevya.
Shuhuda wa tukio hilo (jina linahifadhiwa), alisema watu watatu waliingia ndani ya baa hiyo wakiwa kama wateja na kuanza kutoa ofa za vinywaji na biskuti na kwamba yeye aliondoka baada ya muda kufika na kwamba alipata taarifa kuwa baada ya kula vitu hivyo, walilala wakiwa hoi.
Alisema baada ya kuzidiwa kutokana na kulewa, watu hao watatu walianza kuwabaka wanawake hao hata kufikia hatua kuwaingilia kinyume cha maumbile kisha kupora fedha ambazo thamani yake haijafahamika na kwamba asubuhi alipokuwa anapita, aliona msamaria mwema amewabeba na kuwapeleka hospitali akipitia polisi.
Malema, mmiliki wa nyumba hiyo, alisema ilikuwa usiku wa saa tano waliingia watu watatu kama wateja na mlinzi alifunga geti kutokana na muda kuwa ulikwisha, hivyo walianza kunywa pombe na kuwapa ofa wahudumu pamoja na mlinzi ambaye alipewa soda na biskuti.
Alisema baada ya hapo, wahudumu walilala fofofo, ndipo watu hao wakafanya unyama huo na kwamba hajafahamu kama walibakwa au la kwa kuwa bado wamelazwa katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Mbeya wakiwa hawajitambuhi wakipumulia mashine.
Malema ambaye pia ni diwani wa viti maalumu katika kata ya Manga, alisema wakati anapita aliona msamaria mwema anawabeba ndipo katika kuchunguza akabaini kuwa vijana wake waliingiliwa na watu hao. Alisema alikwenda polisi akapewa barua kwa ajili ya matibabu.
Alisema alipofika baa alikuta fedha zote zimechukuliwa na zikiwamo pia na za upande wa gesti na kwamba hajajua kiasi cha fedha kwa kuwa hawakufunga hesabu. Aliliomba jeshi la polisi kufuatilia kwa kina suala hilo kwa kuwa vijana wake (majina yanahifadhiwa) wamelazwa hospitalini pamoja na mlinzi aliyemtaja kwa jina la Dickson.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei, alisema hajapelekewa taarifa juu ya tukio hilo na mkuu wa polisi wilaya na kwamba atahitaji apate taarifa hizo ili kujua undani wake sambamba na kuweka mikakati ya watuhumiwa ili wakamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya dola.
Credit: Nipashe
Advertisements