Hatma ya ubunge wa Tundu Lissu itajulikana kuanzia Januari 29 wakati Job Ndugai atakapovaa “joho” la uspika kuongoza Mkutano wa 14 wa chombo hicho cha kutunga sheria.
Ndugai amemtaka Lissu arejee nyumbani kuendelea na majukumu yake ya kuwawakilisha wananchi wa Singida Mashariki, akisema hana kibali baada ya mbunge huyo kutoa tamko mwishoni mwa wiki akituhumu kuwepo na mpango wa kumvua ubunge.
Lissu yuko nchini Ubelgiji kumalizia matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 akiwa ndani ya gari, nje ya makazi yake Area D mjini Dodoma, ikiwa ni saa chache baada ya kuhudhuria kikao cha Bunge.
Baada ya shambulio hilo la Septemba 7, mwaka juzi alipelekwa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kabla ya kusafirishwa kwa ndege kwenda Nairobi, Kenya usiku wa siku hiyo.
Mkutano huo wa 14 wa Bunge la Kumi na Moja utaanza Januari 29, siku saba kuanzia leo, pamoja na mambo mengine unatarajiwa kupokea ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), aliyehojiwa jana na Kamati ya Maadili, Haki na Madaraka ya Bunge.
Majibizano kati ya Lissu na Spika Ndugai yamekuwa yakipamba moto siku hadi siku tangu alipotoa waraka alioupa jina la “Baada ya Risasi Kushindwa, Sasa Wanataka Kunivua Ubunge”. Katika waraka huo, Lissu anatuhumu uongozi wa Bunge na Serikali kuandaa mpango huo, jambo ambalo Ndugai amesema “ni uzushi”.
Akiongea katika Mahojiano na Gazeti la Mwananchi jana, Spika Ndugai alisema ; “Alipopata matatizo wote tulishuhudia na Bunge lilitimiza wajibu wake katika zile saa chache ambazo ni muhimu katika kuokoa maisha yake. Na hilo lilifanikiwa. Tunatambua kwamba mwenzetu aliumizwa na alikuwa hospitalini.
“Ila sasa hivi tunavyoongea ametoka hospitali yuko huko aliko. Inaelekea ameruhusiwa. Amekuwa akitumia mwanya huo kuzunguka na kuchafua sifa ya nchi yetu. Kwani nani amempa ruhusa?
“Sasa nimwambie tu kwamba sisi tunamuhitaji maana mpaka sasa hajawahi kuniandikia chochote mimi kama kiongozi wake bungeni na wala daktari wake hajasema kitu. Kwa maana hiyo, mimi namuhesabu kama ni mtoro.”
Alipoulizwa sababu za muhimili huo kushindwa kumuhudumia Lissu licha ya familia yake kuandika barua mara nne, Ndugai alijibu kwa kifupi: “Hayo ya nyuma tuyaache. Atakapokuja mwenyewe tutayazungumza.”
Lakini Lissu, ambaye alihojiwa na Shirika la Habari la Uingereza (BBC) katika kipindi cha Hard Talk kilichorushwa jana alikuwa na majibu ya hoja za Spika.
Alisema kama Spika anataka kujua vizuri hali yake, hahitaji kwenda Ubelgiji bali wapo madaktari ambao Ndugai aliahidi kuwapeleka Nairobi kumuona, lakini hajafanya hivyo.
“(Madaktari) Wakifika Ubelgiji, hawahitaji hata kuzungumza na mimi, wataonana na madaktari wangu na kuzungumza hali yangu na hapo Spika atakuwa na nafasi ya kusema nimepona au la,” alisema mwanasheria huyo.
“Mimi niliumizwa mguu na kiunoni, sikupigwa risasi kichwani, kwa hiyo naweza kuzungumza. Nilikwenda BBC nikitokea hospitalini na nikarudi hospitalini mpaka sasa. Kwa hiyo asiseme nimepona wakati yeye si daktari,”alisema Lissu.
Credit: Mwananchi