Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zachary Kakobe amesema kwa miaka mingi Tanzania imekuwa ikiishi kama nchi ya laana kutokana na matunda yake pamoja na tabu zake kuliwa na nchi isiyojulikana.

Askofu Kakobe ameyasema hayo leo Jumanne Januari 22, 2019 katika mkutano wa wachimbaji, wafanyabiashara na wadau wa sekta ya madini nchini unaofanyika jijini Dar es Salaam.
Askofu Kakobe amesema kwa miaka mingi matunda ya nchi ikiwamo madini yamekuwa yakiliwa na mataifa ya nchi nyingine na kuacha mashimo yasiyo na faida kwa nchi.
“Lakini ni jambo la kushukuru kwa sababu Mungu amemuinua shujaa Rais John Magufuli ambaye amekataa kwamba tuachiwe mashimo na urithi wetu wachukue mataifa mengine na suala hili linahitaji ushujaa sana,” amesema.
Amesema ukiingia katika habari za matunda ya nchi kubaki ndani ya taifa husika umetangaza vita ambayo miongoni mwake ni ile ya kiuchumi.
Pia, Askofu Kakobe alizungumzia tabia ya baadhi ya watu wanaopenda kuona Rais Magufuli anapingwa katika kila jambo licha ya kuwa kuna mazuri mengi anayoyafanya, kama waungwana hawatakiwi kupinga kila jambo hata kama wana hoja bali wanapaswa kutafuta mazuri ya kupongeza ili walete hoja.
“Hata Biblia inasema tutangulize yaliyo mema hata kama una hasira naye, hata Yesu Kristo alipokuwa anatoa ujumbe kwa makanisa saba alikuwa anaanza kupongeza mazuri hata kabla ya kuinua jambo lolote la kupinga, atakayekuwa anapinga atakuwa ni mkorofi na hata ukiwa na hoja itakuwa ngumu kusikilizwa,” amesema Askofu Kakobe.
Amesema Mungu ameipendelea Tanzania katika upande wa ugawaji mipaka na kuifanya kuwa nchi yenye kuvutia kwa kuipatia urithi wa aina mbalimbali.
“Hata ukiangalia kule Moshi namna ramani ilivyopindapinda ili kuruhusu Mlima Kilimanjaro uwe wa kwetu,” amesema.
Amesema kwa miaka mingi watu wamekuwa wakiita Tanzania nchi maskini lakini Rais Magufuli amethibitisha kuwa Tanzania ni nchi tajiri yenye uwezo wa kutoa misaada kwa nchi nyingine.
“Mimi nafikiri unapoanza kupambana na suala hili, uanze kufanyia kazi kwanza fikira za mtu. Kadiri tunapozidi kutamka vitu vizuri ndiyo tunazidi kuvichochea,” amsema.
Advertisements