Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) limeeleza kuwa limepiga maeneo yenye wapiganaji wa Iran ndani ya Syria ambapo majeshi ya nchi hizo na washirika wake yamekutana.

IDF imeeleza kuwa imefanya oparesheni maalum ya kijeshi kulenga wapiganaji wa kundi la Quds ambalo linafanya kazi kwa ushirika na Jeshi la Mapinduzi la Iran (Iranian Revolutionary Guards).
Hata hivyo, Jeshi hilo la Israel halikutoa maelezo zaidi kuhusu madhara yaliyopatikana, lakini limeeleza kuwa maeneo waliyoyapiga alfajiri ya leo ni sehemu ya mji mkuu wa Syria, Damascus.
Hata hivyo, vyombo vya habari vya Syria vimeripoti kuwa kikosi cha anga cha nchi hiyo vimezuia mashambulizi ya Jeshi la Israel katika maeneo ya Damascus nchini Syria.
Shirika la Habari la Syria limekikariri chanzo kimoja cha jeshi kikieleza kuwa vikosi vya nchi hiyo vilidungua makombora kadhaa yaliyokuwa yamerushwa na Israel.
Mashuhuda waliokaririwa na Reuters wameeleza kuwa walisikia milio ya makombora katika maeneo kadhaa ya Damascus.
Hatua hiyo ya Israel imekuja ikiwa ni miezi kadhaa baada ya kueleza kuwa majeshi ya Iran yamefyatua makombora kwa kutumia ndege zisizo na rubani yakilenga vikosi vyake kwenye eneo la Golan.
Waziri Mkuu, Benjamin Netanyahu alipozuru Chad Jumapili alionya kuwa vikosi vya nchi yake vitashambulia vikosi vya Iran nchini Syria kujibu mashambulizi ambayo alidai yalifanywa awali na hao mahasimu wao.
“Tumeandaa sera, kulenga vikosi vya Iran nchini Syria, na kuwadhuru wale wote wanaotaka kutudhuru,” alisema Netanyahu.
Israel imekuwa ikipinga hatua ya Iran kupeleka majeshi yake Syria kwa lengo la kumsaidia Rais Bashar al-Assad ambaye amekuwa wakipambana na vikosi vya waasi vyenye itikadi kali tangu mwaka 2011.
Advertisements