Mahakama Kuu Tanzania imekataa kuipokea kesi ya kikatiba dhidi ya Spika wa Bunge, Job Ndugai kupinga uamuzi wa kumwita Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad katika kamati ya bunge ya haki, kinga na madaraka ya bunge.

Mahakama hiyo imekataa kuipokea na kuisajili kesi hiyo huku ikieleza kuwa ina kasoro za kisheria kutokana na hati za viapo vya wadai wanne pamoja na hati ya wito wa Spika Ndugai na hati ya kiapo cha CAG kutokuambatanishwa kwenye hati ya maombi.
Kesi hiyo ilitarajiwa kufunguliwa na wabunge watano kutoka vyama vitatu vya upinzani wakiongozwa na kiongozi wa ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe.
Wengine ni mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema), mbunge viti maalum Shinyanga Mjini, Salome Makamba (Chadema), mbunge wa Mchinga, Hamidu Bobali (CUF) na mbunge wa Moshi Vijijini, Anthony Komu (Chadema).

Walichukua uamuzi huo baada ya Spika Ndugai kupitia vyombo vya habari na baadaye kumwandikia barua CAG akimtaka afike mbele ya kamati hiyo ya bunge kuhojiwa kutoka na kauli yake aliyoitoa akiwa Marekani kuwa bunge la Tanzania ni dhaifu.
Katika kesi hiyo wabunge hao walikuwa wanaiomba Mahakama itoe tafsiri ya kinga ya CAG iliyopo kikatiba na pia kutoa tafsiri ya sheria ya haki, kinga na madaraka ya bunge katika kushtaki watu wanaosemekana kudharau bunge.