Gazeti la New York Times limeshutumiwa vikali na Wakenya kwa kuchapisha picha za miili ya watu waliopoteza maisha katika shambulio la hoteli ya kifahari ya DusitD2 jijini Nairobi.
Wahalifu wenye silaha za moto na mabomu walivamia viunga vya hoteli hiyo jana Jumanne saa 9 alasiri.
Gazeti hilo lenye makao makuu yake nchini Marekani limechapisha picha za marehemu wakionekana dhairi kuwa na matundu ya risasi kwenye miili yao na kulowa damu.
Baada ya shutuma hizo kushika kasi, uongozi wa gazeti hilo ulitoa taarifa ya kujitetea wakisema lengo lao ni “kuonesha uhalisia wa tukio zima japo picha zinaweza kuwa za kuogofya.”
Maelezo hayo pia yamepingwa, huku Mhariri wa Biashara wa BBC kanda ya Afrika, Larry Madowo akilitaka gazeti hilo kuonesha mifano ya picha za marehemu walizozichapisha kwenye shambulio lolote lililotokea nchini Marekani.
Advertisements