Naibu Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, Jesca Kishoa, amemtaka Spika Job Ndugai, kumwita mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kwa kulidanganya na kulipuuza Bunge kuhusu mkataba kati ya Songas na serikali aliodai ni mbovu.
Songas ni kampuni ya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi iliyoingia mkataba na serikali kuzalisha nishati hiyo kwa kipindi cha miaka 20 kuanzia mwaka 2004.
Imeelezwa kuwa gharama ya mradi wa Songas ni Euro milioni 392. Kati yake, Tanzania ilitoa Euro milioni 285.7 (asilimia 73 ya mradi mzima) na kampuni hiyo ilitoa Euro milioni 106.3.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma jana, Kishoa ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), alisema mkataba huo umekuwa ukilalamikiwa na unaendelea kuisababishia hasara kubwa serikali.
Alisema alipeleka hoja kuhusu suala la Songas bungeni na AG alisimama na kujibu hoja hiyo, akiahidi kutoa taarifa ndani ya miezi miwili tangu Mei 5, mwaka jana, lakini hadi sasa hakuna majibu.
“Katiba ya Tanzania imeeleza mamlaka ya Bunge na ni mhimili mkubwa kushinda wowote, lakini kwa bahati mbaya tumekuwa na viongozi wa serikali ambao wamekuwa wakilidharau na kupuuza Bunge kwa kiwango kikubwa na hawachukuliwi hatua,” alisema.
Mbunge huyo alisema badala ya Spika kumtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Assad, kufika mbele ya Kamati ya Maadili, anafikiri kiongozi wake huyo alipaswa aanze na AG ambaye amepuuza kufuatilia kitu cha msingi, ambacho serikali inapoteza fedha nyingi.
“AG aliahidi ndani ya Bunge na ‘Hansard’ (taarifa za kumbukumbu za Bunge) ninayo tangu mwezi Mei mwaka jana kuwa atafuatilia suala la mkataba wa Songas na kulifanyia marekebisho ndani ya miezi miwili, tulitegemea Julai mwaka jana kila kitu kitakuwa kizuri, lakini hadi sasa hakuna lililofanyika,” alisema.
Kishoa alisema AG ameshindwa kutimiza wajibu wake na kwa mazingira ya aina hiyo, haiwezekani kuzuia watu kuita Bunge ni dhaifu.
“Haiwezekani mtu kutoa ahadi za uongo mbele ya kiti cha Spika, siyo nje ya nchi, kwamba anakwenda kushughulikia suala la Songas kwa kuwa hili suala lipo ‘very complex’ (lina utata), lakini hadi sasa hakuna kilichofanyika,” alisema.
Naibu waziri kivuli huyo alidai kuwa, tangu kuanza kwa mradi huo mwaka 2004 hadi 2018, serikali imepoteza zaidi ya Sh. trilioni 1.3.
“Ifahamike kwamba mkataba huu ni wa miaka 20, mwisho 2024, kama serikali itapuuza, basi tutegemee kupoteza zaidi ya Sh. trilioni mbili kwa kipindi cha utekelezaji wa mradi,” alisema.
Kishoa aliongeza: “Kilichotufikisha hapa ni udhaifu wa Bunge, kwa kuwa ufisadi huu umewahi kuzungumzwa na Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini chini ya Mwenyekiti William Shelukindo mwaka 2005.
“Pia Ripoti ya CAG Ludovick Utoah ya mwaka 2009, Ripoti ya CAG Prof. Mussa Assad ya mwaka 2018 na mimi nimezungumza bungeni mara tatu, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa na Bunge,” alisema.
Mbunge huyo alidai ufisadi huo upo katika maeneo matatu ambayo ni mfumo wa uwekezaji na umiliki, mkataba na gharama za uendeshaji.
“Serikali inamiliki mradi kwa asilimia 46 peke yake na Songas wanamiliki asilimia 54, kama serikali iliwekeza asilimia 73, iweje Songas wamiliki kiwango kikubwa?” Kishoa alihoji.
Alidai kuwa kwenye gharama za uendeshaji, kila mwezi serikali kupitia Shirika la Umeme (Tanesco) inalipa Dola za Marekani milioni tano (Sh. bilioni 11.55).
Naibu waziri kivuli huyo aliishauri serikali kufungua kesi katika mahakama za kimataifa ili kupata utatuzi kama inaona kuna ugumu kulishughulikia suala hilo ndani ya nchi.
“Kama Rais anaona suala hili ni gumu sana kwenye mikono yake, basi apeleke kesi hii kwenye mahakama za kimataifa ambapo anaweza kupata utatuzi bila ukakasi wowote,” alisema.
Kishoa alidai hasira alizoonyesha Rais kwenye ufisadi wa IPTL, ni vizuri zikaonekana pia katika mkataba huo wa Songas na serikali.