Jeshi la Polisi linamshikilia mkazi wa Kijiji cha Moleti Wilaya ya Kongwa, mkoani hapo, Peter Mgomba (26), kwa madai ya kumuua mama yake mzazi kwa kumchoma kisu tumboni.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto, alisema hayo kwenye mkutano na waandishi wa habari, jiijini hapo jana.
Kamanda Muroto alisema tukio hilo lilitokea Desemba 29, katika Kijiji cha Moleti, Tarafa Mlali, Wilaya ya Kongwa.
Alisema tukio la mauaji linadaiwa kufanyika wakati Mgomba alipomchoma kisu tumboni mama yake mzazi, Anita Mgomba (61) na kusababisha kifo.
Alisema chanzo cha mauaji hayo hakijafahamika, lakini wanaendelea na uchunguzi na utakapokamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.
Hata hivyo, Kamanda Muroto alisema mtuhumiwa anasadikiwa kuwa ni mgonjwa wa tatizo la akili na baada ya kufanya tukio alitoroka, lakini jeshi hilo lilimtafuta na kumtia nguvuni.
Alisema siku ya tukio, Anita alijeruhiwa na kukimbizwa hospitalini, lakini akiwa kwenye matibabu Desemba 30, alifariki dunia.
Advertisements