Hadi kufikia Novemba 2018 washirika wa maendeleo walikuwa wamechangia Sh498.5 bilioni ambayo ni asilimia 54 ya kiasi walichotakiwa kuwa wamechangia katika kipindi hicho.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema katika kipindi cha Julai hadi Novemba 2018, wadau hao walipaswa kuwa wamechangia Sh928.7 bilioni kutokana na ahadi yao kwa Serikali kwamba mwaka wa fedha 2018/19 wangechangia Sh2.67 trilioni.

Akizungumza leo Jumapili Desemba 30, 2018 jijini Dodoma, Waziri Mpango ametaja baadhi ya sababu za kutochangia ni kutokana na masharti na vigezo vinavyowekwa na wadau hao ikiwemo kasi ndogo ya utekelezaji wa miradi.

Waziri amesema Serikali imeliona jambo hilo na imejipanga katika kukabiliana na hali hiyo ikiwemo kubana matumizi na kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato.

Wakati huo huo Waziri Mpango amesema deni la Serikali la Sh49.37 trilioni bado ni himilivu hivyo Watanzania hawapaswi kuwa na hofu kwani halizuii Serikali kukopa.

Advertisements