Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam SACP, Lazaro Mambosasa amemuomba Rais Dkt. John Magufuli kutenga Wilaya ya kipolisi Chanika na Mbweni jijini humo ili kurahisisha shughuli za kiusalama na huduma kwa wananchi wa maeneo hayo.

 
Akizungumza katika kongamano la usalama katika jimbo la Ukonga, mapema leo Julai 25, 2018 Mambosasa amesema uhitaji wa Wilaya hizo za kipolisi ni muhimu kwani maeneo hayo yanahitaji kuongezewa askari polisi hadi kufikia 100 lakini kutokana na kuwa hakuna Wilaya ya kipolisi ni ngumu kuongezewa askari hao.
 
“Jambo hili la kukosekana kwa wilaya za kipolisi katika maeneo haya linapelekea shughuli za kiusalama kushindikana huku wananchi wakikosa huduma za kipolisi ngazi ya wilaya na kulazimika kusafiri mwendo mrefu kutafuta huduma hizo”, amesema Mambosasa.
 
Aidha, SACP Mambosasa amewaagiza makamanda wote kusimamia kikamilifu vikundi vya ulinzi shirikishi katika maeneo yao kwani vikundi hivyo vinasaidia kupunguza upungufu wa askari polisi, huku akihimiza kero zote za kata zitatuliwe ngazi ya kata kuliko kuwaacha wananchi kuwa na kero nyingi.
 
Takwimu za matukio ya uhalifu kutoka jeshi la polisi zinaonyesha kuwa katika maeneo hayo kuanzia mwezi Januari, mwaka 2018 kuna matukio ya uhalifu 990 huku ubakaji ya kiwa 89, matukio ya wizi wa pikipiki 154.
Advertisements