Mkurugenzi wa Tume ya Taifa Uchaguzi (Nec), Athuman Kiamia, amesema atavitendea haki vyama vyote vya siasa bila upendeleo wowote.
Amesema atahakikisha sheria, kanuni na miongozo iliyowekwa kuongoza Nec inafuatwa kwa uhalisia.
Aliyasema hayo jana kwenye mkutano baina ya Nec na viongozi wa vyama vya siasa, kuelekea uchaguzi mdogo wa Jimbo la Buyungu, na madiwani kwenye kata 79 za Tanzania Bara unaotarajia kufanyika Agosti 12, mwaka huu.
“Tume inaongozwa na sheria, kanuni na miongozo kwa hiyo mimi Mkurugenzi wa Nec nitahakikisha taratibu zote zinafuatwa kwa uhalisia wake, tutaendelea kuhakikisha haki inatendeka kwa makundi yote,” alisema Athumani.
Alisema pia atahakikisha anashirikiana na menejimenti ya Nec, wajumbe, Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti ili kila kitu kifanyike kwa wakati na haraka.
Athumani amechukua nafasi ya Ramadhan Kailima, aliyeteuliwa na Rais John Magufuli kuwa Naibu Katibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani.
Kuhusu suala la mawakala, Mkurugenzi huyo mpya alisema Nec inatendelea kutoa elimu kwa vyama vya siasa kwa kuwa suala hilo limekuwa likileta mtafaruku mara kwa mara.
“Vyama vya siasa muhimu wazingatie muda wa uapishwaji, na uletwaji wa majina ya mawakala ufanyike siku saba kabla ya siku ya uchaguzi.”
“Wajibu wa mawakala na wasimamizi wa uchaguzi ukizingatiwa hakutakuwa na changamoto,” alisema Athumani.
Alisema kama alivyoweza kusimamia uchaguzi katika Jiji la Arusha alipokuwa Mkurugenzi kwa kusimamia kufanyika kwa uchaguzi mdogo marambili bila ya kuwapo kwa malalamiko.
Alisema atachanganya uzoefu alioupata katika Jiji la Arusha na maeneo mengine kuimarisha Nec.
Advertisements