Kamati ya Bunge iliyoundwa na Spika Job Ndugai kuchunguza mapato yatokanayo na gesi asilia imependekeza mkataba wa Songosongo usihuishwe mara utakapofikia mwisho wake mwaka 2024.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumamosi Juni 2, 2018 na mwenyekiti wa kamati hiyo, Dunstan Kitandula wakati akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo katika hafla fupi iliyofanyika katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma.
Amesema kuwa mkataba huo namna ulivyo hauna faida kwa Serikali, badala yake umeegemea upande mmoja wa mwekezaji.
Kitandula amesema mkataba huo unamalizika mwaka 2024 na kwamba hadi sasa kamati yake ina amini kuwa mwekezaji alisharudisha gharama zake.
“Pamoja na hayo, tunapendekeza kuwa wahusika wote katika miradi ya gesi ikiwemo mradi kuchunguzwa na vyombo vya ulinzi na usalama ili kuona kama walikuwa na nie njema na nchi yetu au la,” amesema Kitandula.
Amesema kuwa inashangaza kuona baadhi ya watumishi walioliingiza Taifa kwenye mikataba hiyo ya utata bado wapo ndani ya Serikali wakiendelea na utumishi.
Advertisements