KAMA ni mpenzi wa Muziki wa Taarab kwa muda mrefu ni wazi utakuwa umezisikia nyimbo nyingi za muziki huo kutoka makundi mbalimbali.

Kundi la JKT Taarab ni miongoni tu mwa makundi yaliokuwa yakitisa katika muziki huo kipindi yupo mwanamuziki mkongwe, Marehemu Nasma Khamis Kidogo.

Ukiachilia mbali Wimbo wa Mahaba ya Dhati na Mtu Mzima Hovyo zilizompa umaarufu, Subalkheri Mpenzi nao ni kati ya nyimbo zilizokuwa ngumu kukauka kwenye midomo ya wapenda Taarab.

Wakali wawili wanaounda ‘chemistry’ ya ajabu kwenye Muziki wa Bongo Fleva, Nandy na Aslay wamech-ungulia nyimbo za Nasma na kufanikiwa kuunasa wa Subalkheri Mpenzi kisha kuufanyia kazi Kibongo-flevafleva na ukatoka bomba mbaya!

Katika makala haya, huyu hapa Nandy anaufungukia zaidi wimbo huo na maisha yake ya kimapenzi kwa ufupi huku akianika siri za msanii mwenzake, Aslay;

Over Ze Weekend: Katika wimbo wenu mpya wa Subalkheri Mpenzi uliotoa na Aslay unaweza kutuambia nani amemshirikisha mwenzake?

Nandy: Huo ni wimbo wa wote hakuna aliyeshirikishwa.

Over Ze Weekend: Lakini tunajua kuwa uliwahi kuimbwa kabla na mkongwe wa Taarab, marehemu Nasma Khami

 

Kidogo kipindi akiwa JKT Taarab, je, mlimshirikisha?

Nandy: Yah! Uongozi wetu uliamua kufanya kila kitu na kutukabidhi tuimbe tu.

Over Ze Weekend: Ilikuwaje sasa uongozi wako huo ukaona kama ukitoa wimbo huo na Aslay utapendeza?

Nandy: Aslay nilianza kufanya naye Wimbo wa Mahabuba na mashabiki wakapenda na kuhitaji kufanya naye kazi nyingine zaidi.

Over Ze Weekend: Katika ngoma zako zote ulizowahi kushirikishwa, huu Subalkheri Mpenzi umechukuliwaje na mashabiki wako?

Nandy: Ni wimbo mkubwa kiukweli umepokelewa vizuri.

Over Ze Weekend: Tunajua Aslay ana uongozi wake na wewe hivyo lakini umesema kuwa Wimbo wa Subalkheri Mpenzi uongozi wenu ndiyo umeubariki, hii ipoje?

Nandy: Tunafanya kazi pamoja na uongozi wake na wangu upo pamoja.

Over Ze Weekend: Mashabiki wengi wanahisi kama upo katika uhusiano na Aslay licha ya kuimba naye, unaweza kufafanua hili?

Nandy: Hapana bwana! Hata mimi hizo habari nazisikia lakini nafanya kazi yangu ya muziki.

Over Ze Weekend: Mbali na muziki, umekuwa ukifanya mitindo ya nguo kwa kuwavalisha viongozi mbalimbali nchini, vipi bado unaendelea nayo?

Nandy: Bado naendelea na nguo nyingi zinaonekana na duka langu bado lipo linafanya biashara.

Over Ze Weekend: Katika kuimba na kucheza Wimbo wa Subalkheri Mpenzi umeonekana kukupa wakati mgumu hata kwenye maandalizi ya video, ilikuchukua muda gani kuiweza Taarab?

Nandy: Yaani ni kweli! Nilikuwa najaribu kukopi hadi nikaweza, sikupata saaana ugumu lakini ilikuwa wa kawaida tu.

Over Ze Weekend: Kimuziki kwa sasa unaonekana upo juu na kufanikiwa kuwafunika baadhi ya wanamuziki uliowakuta. Hebu tuambie urafiki wako na msanii mwenzako, Ruby kwa sasa upoje?

Nandy: Yah tupo poa ni watu tu wanavyoona lakini hatuna tatizo.

Over Ze Weekend: Hebu tunaomba utupe ukweli kuhusu hawa watu, Billnas na Dogo Janja.

Nandy: Heee heee! Hapo kama sijaelewa!

Over Ze Weekend: Tunataka kujua kama una uhusiano wa kimapenzi na Billnas wakati huohuo na Dogo Janja inadaiwa upo naye?

Nandy: Billnas ni mshikaji wangu lakini Dogo Janja ni mshkaji saaana ambaye nipo naye free sana.

Over Ze Weekend: Tangu umekuwa karibu kimuziki na Aslay tunajua umepitia naye mengi, vitu gani unavipenda kutoka kwake?

Nandy: Ngoja nikupe siri, namkubali sana Aslay kwa sababu ni mtu wa vitukovituko sana halafu ana heshima ya kazi.

Over Ze Weekend: Nyimbo zako nyingi za mapenzi na hisia, hujawahi kupata usumbufu kwa wanaume wakware?

Nandy: Usumbufu naupata lakini ni wa kawaida.

Advertisements