Mgogoro  ndani ya Chama cha Wananchi (CUF) bado unafukuta ambapo jana Prof. Ibrahim Lipumba, aligomea mkutano wa Baraza Kuu la Uongozi la chama hicho ulioitishwa leo visiwani Zanzibar
Alisema, taarifa zilizotolewa kwa vyombo vya habari kuhusu kufanyika kwa mkutano huo hazitambui kwa kuwa, mamlaka zinazohusika kuitisha kikao hicho hazijakidhi matakwa.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi Kuu ya chama hicho Buguruni jijini Dar es Salaam kupitia taarifa iliyoandaliwa na Magdalena Sakaya, Naibu Katibu Mkuu Bara aliyesimamishwa na chama hicho alisema, matakwa ya katiba hayakuzingatiwa.
“Wajibu wa Kamati ya Utendaji ya Taifa utakuwa kuandaa.. agenda za Baraza Kuu la Uongozi la Taifa na kutayarisha na kuhifadhi mihtusari ya vikao vyote vya Mkutano Mkuu wa Taifa, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa na vya kamati ya utendaji ya taifa yenyewe na kuwasilisha taarifa ya yatokanayo kutokana na utekelezaji wa maamuzi ya kikao kilichohusika kilichopita,” Prof. Lipumba amenukuu katiba ya chama hicho ibara ya 85(5).
Prof. Lipumba alisema, Maalim Seif Shariff Hamad, Katibu Mkuu wa chama hicho yupo nje ya nchi na kwamba, kutokana na Katiba ya CUF,Naibu Katibu Mkuu atakayemfuata Katibu Mkuu kwa madaraka ni yule aliyetoka upande tofauti wa Jamhuri ya Muungano na upande anaotoka Katibu Mkuu
Kwa upande wake Magdalena Sakaya, Naibu Katibu Mkuu Bara aliyesimamishwa alisema;
“Mimi sijaitisha wala sina taarifa ya kikao cha kamati  ya utendaji kilichofanyika Zanzibar, kwa taarifa nilizonazo hakuna wajumbe wa kamati ya utendaji kutoka Bara waliokua Zanzibar wakati wa kikao hicho. Nachukua nafasi kuwajulisha wajumbe wote wa baraza kuu kuwa hakuna kikao chochote cha baraza kuu kilichoandaliwa na kamati ya utendaji ya Taifa ambayo kikatiba mimi ndiye mwenyekiti wake wakati katibu mkuu hayupo.
“Mimi ndiye mwenye mamlaka ya Katibu Mkuu kwa sababu Naibu Katibu Mkuu wa CUF Tanzania Bara kikatiba ndiye msimamizi namba moja wa Katibu Mkuu” .
Alisema, Katiba ya CUF ya mwaka 1992 Toleo la 2014 kifungu cha 95 (3) kinaeleza “Naibu Katibu Mkuu atakayemfuata Katibu Mkuu kwa madaraka ni yule aliyetoka upande tofauti wa Jamhuri ya Muungano na upande anaotoka Katibu Mkuu,” na kwamba, Katibu Mkuu anatoka Zanzibar na yeye anatoka Bara.
Hata hivyo Prof. alisisitiza kuwa, Sakaya hana taarifa ya kikao hicho cha kamati tendaji kilichofanyika Zanzibar.
Pamoja na kuwepo kwa sintofahamu kutokana na uamuzi wa Jaji Mutungi kumtambua Prof. Lipumba kuwa mwenyekiti halali wa chama hicho, (Lipumba) amepongeza kurejeshwa kwake.
Prof. Lipumba, mwenyekiti wa chama hicho aliyesimamishwa na CUF mwezi uliopita, alirejea kwenye nafasi hiyo kwa kauli ya Jaji Mutungu, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini.
Prof. Lipumba alieleza kushangazwa na hatua ya Jaji Mutungi kukosolewa na baadhi ya wanasheria na majaji mashuhuri kuwa, hakuna sheria inayompa furasa jaji huyo kuchukua hatua aliyoichukua.
Advertisements